Thursday, September 18, 2014

SIMULIZI TAMU YA KHADIJA KOPA

1 Comment
BAADA ya wiki iliyopita kumaliza simulizi tamu ya mwimba Injili mahiri nchini, Bahati Bukuku, wiki hii tunaye malkia wa mipasho Bongo. Si mwingine bali ni Hadija Omar Kopa.
Malkia wa mipasho Bongo, Hadija Omar Kopa akiwa kazini.
Kopa alizaliwa mwaka 1963, Unguja, Zanzibar. Maisha yake yalikuwa ya kawaida sana. Kwa sehemu kubwa alilelewa na bibi yake mzaa mama, aitwaye Biubwa Juma. Katika simulizi hii, Kopa anaanza kusimulia siku alipoanza daraza la kwanza.
Twende naye…
BAADA ya wiki iliyopita kumaliza simulizi tamu ya mwimba Injili mahiri nchini, Bahati Bukuku, wiki hii tunaye malkia wa mipasho Bongo. Si mwingine bali ni Hadija Omar Kopa.
Malkia wa mipasho Bongo, Hadija Omar Kopa akiwa kazini.
Kopa alizaliwa mwaka 1963, Unguja, Zanzibar. Maisha yake yalikuwa ya kawaida sana. Kwa sehemu kubwa alilelewa na bibi yake mzaa mama, aitwaye Biubwa Juma. Katika simulizi hii, Kopa anaanza kusimulia siku alipoanza daraza la kwanza.
Twende naye mwenyewe...
Siku hiyo nilijikunyata kitandani, kazi yangu kubwa ilikuwa ni kuvuta shuka na kuufunika mwili wangu vilivyo. Baridi lililokuwa likinipiga asubuhi ya siku hiyo lilikuwa kubwa, ni zaidi ya siku zote katika ardhi ya Zanzibar.
Wakati macho yangu yakiwa mazito tena huku nikiwa nimelishikilia vizuri shuka langu zito, nikasikia sauti ya mama ikiniita. Sikutaka kuamka japokuwa niliisikia vilivyo sauti yake, nilichokifanya ni kulivuta vizuri lile shuka zito na kuendelea kuuchapa usingizi.
Aamshwa na mama yake akaanze shule
Ghafla, mlango ukafunguliwa na mama kuingia. Siku hiyo alikuwa tofauti na siku nyingine, alionekana mwenye haraka, akanifuata kitandani na kunitaka niamke.
Nahisi huo ndiyo ulikuwa mtihani mgumu kwangu, kuamka kitandani na wakati kulikuwa na baridi, lilikuwa jambo gumu.
“Amka Hadija, nitakuchapa,” aliniambia mama.
Huku nikiwa nimekasirika, nikaamka na kuanza kumwangalia. Alinionea huruma mno kwani macho yangu yalionesha kwamba nilikuwa na usingizi mzito ambao haukuwa umekwisha.
Mama alinibeba na kunipeleka nje kunawa. Mawingu mazito yalikuwa yametanda huku manyunyu ya mvua yakiendelea kudondoka, mvua kubwa iliyonyesha toka usiku uliopita, muda huo ndiyo ilikuwa imepungua.Mama yangu kipenzi, Bi.
Zuhura Juma Ali akaanza kuninawisha. Mpaka kufikia hapo sikujua ni kitu gani kilimfanya mama kunifuata nyumbani hapo siku hiyo kisha kuninawisha Ilionekana kwamba alitaka twende sehemu.
Alilelewa na bibi
Naomba nikwambie kitu. Maisha yangu ya utoto sikulelewa na mama, niliishi na bibi aliyeitwa Bi. Biubwa. Nilimchukulia kama mama.
Mama alikuwa akifika mara chache kunijulia hali, kama kulikuwa na matumizi yaliyokuwa yakihitajika alitoa kiasi cha fedha na kuondoka zake.
Hiyo ilikuwa mwaka 1971 huko Zanzibar. Hakukuwa na maendeleo makubwa kama ilivyo sasa na hata sehemu kubwa haikuwa imejengwa kama sasa.
“Tunakwenda shule, unakwenda kuanza masomo,” aliniambia mama.
Kwanza nikashtuka, mwili wangu ukanyong’onyea na kuanza kumwangalia usoni. Ni kweli kwamba nilitamani kusoma katika kipindi hicho nilichokuwa na miaka nane, tatizo lililokuwepo ni kwamba, niliogopa fimbo.
Marafiki zangu waliokuwa wakisoma waliniambia shuleni kulikuwa na fimbo hivyo kunifanya kuogopa mno. Sikutaka kusoma kwa sababu hiyo. Nilitamani kumkatalia mama, lakini sikuwa na jinsi.
“Twende ukavae tuondoke,” mama aliniambia.
Nakumbuka siku hiyo hata kuoga sikuoga. Kulikuwa na baridi kali, mama alilifahamu hilo hivyo akaogopa kuniogesha kwa kuamini ningeweza kupatwa na vichomi, aliniambia ninawe kisha kuondoka kuelekea shuleni.Njiani sikuwa na furaha, kila wakati niliona kwamba na mimi ilikuwa zamu yangu kuchapwa fimbo kama ilivyokuwa kwa wanafunzi wengine.
Amweleza ukweli mama kuhusu viboko
Sikufichi, siku hiyo nilimwambia mama wazi kwamba naogopa kuanza shule kwa kuwa kulikuwa na viboko.
“Usiogope Hadija, hautochapwa,” aliniambia.
Japokuwa alinitia moyo, aliniondoa hofu lakini moyo wangu uliendelea kukataa kabisa, nilichokuwa nikijua ilikuwa ni lazima nichapwe tu.
Baada ya dakika chache tukafika katika Shule ya Msingi ya Ng’ambo ambayo kwa sasa inaitwa Raha Leo.
Kitendo cha kufika shuleni hapo tu, macho yangu yakatua kwa wanafunzi waliokuwa wakichapwa kwa kuwa walifanya makosa, hofu niliyokuwa nayo nayo ikaongezeka zaidi kwa kuona kwamba hata mimi nilikuwa nimeingia katika mdomo wa mamba, hivyo nisingeweza kunusurika.
Siku hiyo nikaanza masomo yangu shuleni. Sikuwa na furaha kama wengine, nilikuwa mnyonge huku kichwa changu kikifikiria fimbo tu.Siku ya kwanza, sikupata rafiki yeyote, nilikwenda shule na baadaye kurudi nyumbani ambapo bibi alitaka kufahamu nilijifunza nini.
Ashinda mnyonge darasani
Ilikuwa ngumu kumwambia kwani sikusoma zaidi ya masaa yote ya shule kuwa mnyonge. Kwa sababu mama alikuwa ameacha kiasi kidogo cha fedha, hichohicho ndicho kikatumika kununulia madaftari pamoja na sare za shule.
“Ukifika shule, soma sana, tunataka na wewe uje kuwa rais, umesikia Hadija?” aliniambia bibi.
“Nimesikia, nitasoma. Ila naogopa fimbo bibi.”
“Usiogope, hautochapwa.”
“Kweli bibi?”
“Kweli, hautochapwa.”
“Sawa.” Kwa kuwa nilikuwa mdogo, maneno ya bibi nikayaamini kwa asilimia mia moja kwamba nisingeweza kuchapwa, kumbe nilikuwa nikijidanganya tu.
Siku iliyofuata, nikaelekea tena shuleni. Sikuwa na rafiki yeyote, marafiki zangu wengi niliokuwa nao nyumbani walikuwa wakisoma shule za tofauti kabisa na hiyo.

Itaendelea wiki Ijayo.

0 comments: