Monday, September 15, 2014

Mzimu wa Posho Bunge la Katiba Waibuka Tena, Kamati ya Uandishi Wataka Posho ya Sh500,000 Kwa Siku

Mzimu wa posho umeibuka upya katika Bunge la Katiba, safari hii wajumbe wake wa Kamati ya Uandishi wakiomba walipwe posho maalumu ya Sh500,000 kwa siku kutokana na kazi ya kuandika Rasimu ya Katiba inayopendekezwa.

Habari zilizolifikia Mwananchi na kuthibitishwa na uongozi wa Bunge zinasema kuwa tayari maoni ya wajumbe yamewasilishwa kwa uongozi kwa ajili ya uamuzi.

Wajumbe wa kamati hiyo kwa sasa wanalipwa posho maalumu ya Sh210,000 zaidi kwa siku, nje ya ile ya Sh300,000 kwa siku wanayolipwa wajumbe wote wa Bunge hilo.

Kamati hiyo inayoongozwa na Andrew Chenge ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi Magharibi-CCM inahusisha baadhi ya vigogo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Vigogo hao ni pamoja Waziri wa Sheria na Katiba, Dk Asha-Rose Migiro, Mwanasheria Mkuu Jaji Frederick Werema, Mwanasheria Mkuu wa SMZ, Othman Masoud Othman aliyejiuzulu ujumbe wa kamati hiyo hivi karibuni kwa sababu ambazo hazijaelezwa.

Katibu wa Bunge, Yahaya Khamis Hamad pamoja na kukiri kuwa kamati hiyo imeomba kuongezwa kiasi hicho cha posho, alisema Kamati ya Uongozi ambayo ndiyo huamua, haijayajadili maombi hayo na kuyatolea uamuzi.

Chenge hakupatikana jana kuzungumzia maombi hayo.
                                www.2dayhabari.blogspot.com

0 comments: