Uwekezaji ulivyoua Mji wa Mirerani-2
SheikhMohammed anasema serikali ndio inawanyanyasa wananchi wake kwa kupitisha sheria ambazo zinawazuia kunufaika na rasilimali za taifa lao ambazo Mungu amewapa.
“Wachimbaji wadogo wamepewa migodi yenye ukubwa wa
mita 50 kwa 50 lakini mchimbaji mmoja mkubwa amepewa eneo kubwa zaidi
ya eka tano halafu inapitishwa sheria ya kuchimba kwenda chini jambo
ambalo haliwezekani huku ni kuwazuia wachimbaji wadogo kupata madini”
alisema.
Alisema kwa sasa shughuli nyingi za msikiti huo
zimesimama kwani wananchi wa Mirerani hawana fedha za kutoa sadaka
tofauti na miaka ya nyuma ambapo sadaka ziliwezesha ujenzi wa msikiti
huo, shule na kuwa na miradi.
Padri Aloyce Kitomali wa Kanisa la Katoliki
Mirerani, alisema kanisa hilo lilikuwa na uwezo wa kukusanya sadaka
katika ibada moja zaidi ya milioni moja lakini sasa hata Sh500, 000
hazipatikani kwani waumini hawana fedha.
Anasema miradi mingi ya kanisa hilo, sasa
imezorota kwani wananchi wengi wanategemea madini ya tanzanite ambayo
sasa hayapatikani na inasemekana anayepata ni mwekezaji.
“Wananchi hapa wengi wana hali ngumu ya maisha
tofauti ya miaka ya nyuma kwani uchumi wao ulitegemea sana madini ya
Tanzanite” alisema.
Osca Gunewe ambaye ni Katibu wa Bodi ya shule ya
Kanisa la Pentekoste, anasema uchumi wa mji wa Mirerani unategemea
madini ya Tanzanite hivyo kwa hali iliyopo sasa ni muhimu Serikali
kuwasaidia wakazi wa mji huo.
Gunewe ambaye aliwahi kuwa Ofisa Mtendaji wa Kata
ya Mirerani, anasema ingewezekana kuwasaidia watu wa Mirerani hata kwa
kutolewa ajira kwa vijana wa Mirerani katika migodi ya mwekezaji.
Anasema lakini kampuni hiyo, haiajiri vijana wa
Mirerani na hivyo sasa wapo mitaani tu kwani hata migodi ya wachimbaji
wadogo mingi imesimama na ambayo inaendelea na kazi, inachukua vijana
wachache sana.
Omar Awadhi alikuwa Mwenyekiti wa Serikali ya
Kijiji cha Mirerani miaka 10 iliyopita, anasema, maisha ya Mirerani sasa
yamebadilika na hata uchangiaji shughuli za maendeleo umepungua sana.
Anasema Mirerani licha ya utajiri wote, haina hata huduma ya maji safi,
kwani ndoo moja inauzwa kati ya Sh400 na 500.
Awadhi anasema maji hayo yanatolewa Wilaya ya Hai
Mkoa wa Kilimanjaro kitu ambacho siyo sahihi kulingana na utajiri wa
tanzanite ambayo inapatikana Mirerani pekee duniani.
“Tatizo hapa ni mwekezaji kama madini haya
yangechimbwa na wachimbaji wadogo pekee hali isingekuwa hivi, kwani watu
wengi wangepata madini japo kidogo kidogo lakini yangeendelea kuujenga
Mji wa Mirerani na hata mikoa ya jirani,” anasema.
0 comments: