Thursday, August 28, 2014

SIMULIZI TAMU YA BAHATI BUKUKU-12


ILIPOISHIA:

Iliishia pale Bahati alipokuwa na kiu ya kuolewa, alipiga goti na kumuomba Mungu kwamba endapo atampa mume, basi awe mume aliyetoka kwake (Mungu). ENDELEA...
Mwimbaji wa nyimbo za injili Bongo, Bahati Bukuku.
Ikumbukwe kwamba siku nimezaliwa katika familia inayomjua Mungu, nimelelewa katika wokovu kwa kipindi chote cha maisha yangu, kwa hiyo hata kwenye suala zima la kuolewa nililiacha mikononi mwa Mungu.
Siku ziliendelea kukatika, bado huduma yangu ya kumuimbia Mugu iliendelea kama kawaida. Wengi…
ILIPOISHIA:
Iliishia pale Bahati alipokuwa na kiu ya kuolewa, alipiga goti na kumuomba Mungu kwamba endapo atampa mume, basi awe mume aliyetoka kwake (Mungu). ENDELEA...
Mwimbaji wa nyimbo za injili Bongo, Bahati Bukuku.
Ikumbukwe kwamba siku nimezaliwa katika familia inayomjua Mungu, nimelelewa katika wokovu kwa kipindi chote cha maisha yangu, kwa hiyo hata kwenye suala zima la kuolewa nililiacha mikononi mwa Mungu.
Siku ziliendelea kukatika, bado huduma yangu ya kumuimbia Mugu iliendelea kama kawaida. Wengi walivutiwa na sauti yangu hasa nilipokuwa nikiimba nyimbo za kuabudu ambazo zilinifanya nijione kuwa karibu sana na Mungu. Wakina dada bado walikuwa wakiolewa kanisani, nilikuwa muhudhuriaji mzuri wa harusi za watu bila kujua kwamba harusi yangu na mimi ilikuwa karibu kuja.
AKUBALIANA KUOANA NA DANIEL
Siku zikakatika mpaka pale nilipompata mwanaume ambaye nilikaa naye chini, tukakubaliana na hatimaye kutangaza uchumba, huyu alikuwa Daniel Basila. Alikuwa kijana mcha Mungu ambaye alikuwa na ukimya fulani kanisani.
Nilipokamilisha kila kitu pamoja naye, nikawaambia wazazi wangu juu ya kijana huyu na wao walionekana kuwa na furaha kwa kuona kwamba nilikuwa nimeingia katika hatua nyingine kabisa ya kuitwa mke wa mtu.
“Unaolewa?” aliniuliza rafiki yangu, Neema.
“Ndiyo. Lakini kwanza itatakiwa kutangaza uchumba,” nilimwambia Neema Simuni, msichana aliyekuwa rafiki yangu kwa kipindi kirefu sana, toka shuleni.
AWATAARIFU WAZAZI
Huku harakati nyingine zikiendelea, nikaamua kuelekea mkoani Mbeya kuwataarifu wazazi wangu kwamba tayari nilikuwa nimepata mwanaume atakayenioa ili hata siku ya kutangazwa kwa uchumba kanisani nao wawepo.
Baada ya siku kadhaa, nikarudi Dar. Sisi watu tuliookoka ni tofauti sana na watu wasiookoka. Tulitarajiwa kuwa wachumba lakini hatukutakiwa kuwa karibu sana. Kulikuwa na vifungo ambavyo huwa tunawekewa mpaka pale vitu vingine vitakapokamilika.
MCHUNGAJI ATANGAZA NDOA
Siku ambayo mchungaji alitangaza kanisani kwamba Jumapili ya wiki ijayo kutakuwa na tangazo la uchumba litatolewa kanisani, kila mtu alikuwa na hamu ya kutaka kufahamu alikuwa nani na nani.
Hakukuwa na mtu aliyejua kwamba mmoja wa watu hao ningekuwa mimi kutokana na heshima niliyojiwekea kanisani na muonekano wangu, nilionekana kama supastaa fulani ambaye sikutakiwa kuolewa na mtu wa kawaida au msichana ambaye nilitakiwa kuolewa na mchungaji.
WAZAZI WAFIKA DAR
Nikawapigia simu wazazi wangu na kuwataarifu kwamba Jumapili ya wiki inayofuatia ilikuwa siku ya kutangazwa kwa uchumba wangu, walifurahi mno na waliniahidi kutua ndani ya Jiji la Dar es Salaam ndani ya siku chache.
Siku ya Alhamisi wakafika nyumbani huku kila mmoja akiwa na furaha, hawakuamini kama binti yao nilikuwa nikitarajiwa kuolewa mwaka huo.
“Daniel yupo wapi?” aliuliza mama huku akionekana kuwa na presha kubwa.
“Yupo, atakuja kututembelea, msijali, kila kitu kikiwa tayari, atakuja tu,” nilimwambia mama ambaye alionekana kuwa na furaha isiyo kifani.
Nadiriki kusema kwamba toka nimezaliwa, sikuwahi kumuona mama akiwa na furaha kubwa kama kipindi hicho.
PETE ZA UCHUMBA ZANUNULIWA
Japokuwa hatukutakiwa kuonana mara kwa mara ila nilikuwa nikiwasiliana na Daniel na kumwambia kwamba ilitakiwa kununua pete kwa ajili ya kuvishana katika siku ya kutangazwa kwa uchumba wetu.
Siku ya Ijumaa, akanitaarifu kwamba tayari pete zilikuwa zimekwishanunuliwa na hivyo nilitakiwa niifuate ile niliyotakiwa kuivaa siku ya Jumapili kanisani. Kuonana haikuwa ikiruhusiwa hivyo nilimtuma ndugu yangu aende huko kuichukua pete hiyo na kuja nayo.
Ndani ya masaa mawili, alikuwa nyumbani hapo huku akiwa na ile pete ambayo kila nilipokuwa nikiiangalia, nilibaki nikiwa na furaha tele.
AKATAA KUVAA PETE NYUMBANI
“Hebu ijaribishe,” aliniambia mama, yeye muda wote tu alikuwa na furaha.
“Hapana. Sitaki.”
“Kwa nini? Hutaki kuolewa?”
“Mama, nataka niivae kwa mara ya kwanza nitakapokuwa kanisani,” nilimwambia mama.
“Jamaniiii, siamini, naozesha kwa mara nyingine,” mama aliwaambia ndugu zangu wengine waliokuwa sebuleni pale.
Siku hiyo, tulikula na kunywa, kila mmoja alionekana kuwa na furaha mno. Kwangu, mawazo yangu yalikuwa siku hiyo tu. Sikuwahi kutangaza uchumba kabla, nilijiona kuwa wa tofauti, nilijaribu kuvuta picha siku hiyo itakuwaje.
Japokuwa mara nyingi nilisimama mbele za watu na kuimba lakini nikajiona nikianza kusikia aibu.
“Nitasimama tu mbele za watu, mbona hata kuwaimbia ninawaimbia na sioni aibu,” nilijisemea na kujipa ujasiri.
UCHUMBA WATANGAZWA RASMI
Siku zilikatika na hatimaye Jumapili kuingia. Siku hiyo, mama yangu na ndugu zangu wengine walikuwa wamejiandaa, walichukua vitenge na zawadi nyingine kwa ajili ya kunitunza kanisani katika siku ya kutangaza uchumba.
Nilipofika kanisani, mapigo ya moyo siku hiyo yalikuwa yakidunda kwa kasi mno, sikutakiwa hata kuongoza kipindi cha sifa, nilitakiwa kutulia kwa kusubiri tukio lililokuwa maalumu katika maisha yangu. Baada ya sifa na kuabudu kumalizika, kipindi cha matangazo kikaingia.
Baada ya matangazo yote kumalizika, mchungaji akakabidhiwa kipaza sauti kwa kuwa alikuwa na tangazo maalumu, hapo, mapigo ya moyo yalidunda kwa kasi mpaka wakati mwingine nikahisi moyo unataka kuchomoka.
“Kooh...kooh...” alianza kwa kukohoa, vigelegele vikaanza kusikika. Kulikuwa na watu, hasa marafiki zangu wa karibu walijua ni kitu gani kilichokuwa kikitaka kutokea na wahusika walikuwa wakina nani, ila pamoja na hayo wote, kuna wale wengine waliokuwa wakijua tukio lakini wahusika hawakuwa wakijulikana.
WAVALISHANA PETE
Hata kabla mchungaji hajatangaza kitu chochote kile, tayari wasichana walikuwa wamekwishasogea kwangu huku wakiwa na khanga mikononi mwao.
“Mbona mmekwenda huko jamani?” aliuliza mchungaji huku akitabasamu, sauti yake ilisikika kiutani. Kanisa zima likaanza kucheka. Siku hiyo uchumba wangu na Daniel ukatangazwa, tukavalishana pete mbele ya kanisa na hatimaye kuingia kwenye uchumba. Kanisa zima lilishangaa na maisha ya uchumba kuanzia hapo.
Kama ilivyo kawaida yetu Wakristo, wachumba hatukutakiwa kuonana mara kwa mara, wakati mwingine nilipokuwa nikienda kumtembelea kwake ilikuwa ni lazima niende na msichana mwingine kwa kuogopa kufanya kitu kingine kwani niliamini kwamba shetani alikuwepo kazini.


Itaendelea wiki ijayo.

0 comments: