Tuesday, August 19, 2014

DIAMOND, WEMA MWISHO UMEFIKA



Stori: Imelda Mtema na Gladness Mallya
Mwisho wa reli? Lile penzi lenye taito na mbwembwe nyingi Bongo kati ya sexy lady wa Bongo Movies, Wema Isaac Sepetu ‘Beautiful Onyinye’ na staa wa Ngoma ya Mdogomdogo, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ linadaiwa kufika mwisho baada ya jamaa huyo kumwandikia mwenziye waraka wa kumdhalilisha mtandaoni, Ijumaa Wikienda lina sarakasi nzima.
Staa wa Ngoma ya Mdogomdogo, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’
TUJIUNGE INSTAGRAM
Suala la Wema kukashifiwa liliibuka baada ya wadau mbalimbali ambao ni mashabiki wa Wema wanaojiita Team Wema kuhoji kwenye Mtandao wa Instagram kwamba ni kwa nini Diamond alimtumia Wema kwa kukata mauno jukwaani (hivi karibuni kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza) badala ya kumfungulia biashara ya maana?
“Tujaribuni kumshauri Wema maana tunaona anatumiwa vibaya na huyu Diamond. Haiwezekani ampandishe kwenye majukwaa halafu amkatishe mauno namna ile kama kweli ana nia ya kumuoa,” aliandika mmoja wa wadau ambaye ni mfuasi wa Team Wema.
Team Wema walidaiwa kufungua mjadala huo wa kumshauri ‘msanii wao huyo wa ukweli’ kufuatia kusambaa kwa picha zinazomuonesha Wema akiwa na shosti wake, Aunt Ezekiel Grayson wakikata mauno jukwaani kupitia wimbo wa Diamond wa Mdogomdogo.
WATOA MIFANO YA WAREMBO
Wadau hao walimtaka Wema kuiga mifano ya warembo wenzake waliopita kama Nancy Sumari (2005), Hoyce Temu (1999), Faraja Kotta (2004) na wengine wengi kwa jinsi wanavyojishughulisha na shughuli mbalimbali na kuweza kuendesha maisha yao bila kudhalilishwa majukwaani.
Sexy lady wa Bongo Movies, Wema Isaac Sepetu ‘Beautiful Onyinye’
WAKERWA WEMA KUWA MCHEZA SHOO WA DIAMOND
Team Wema walikwenda mbali zaidi kwa kusema kwamba, wanasikitishwa na Wema kutojulikana moja kwa moja anafanya kazi gani ya maana, zaidi ya kuwa na uhusiano na Diamond ambaye anamgeuza kama mcheza shoo wake wa kukata mauno.
DIAMOND AWAJIBU
Baada ya wadau hao kumshauri Wema huku wakihoji baadhi ya mambo ambayo walidai yanamdhalilisha, kupitia mtandao huohuo wa Instagram, Diamond alishindwa kuvumilia ushauri huo uliomgusa na kuamua kuandika waraka wake unaodaiwa kumdhalilisha Wema.
Katika waraka huo, Diamond alieleza kwamba yeye kama yeye huwa anamtimizia Wema mahitaji ya muhimu kama mpenzi wake na suala la kumpa mtaji wa kufanya biashara.
WARAKA WENYEWE:
“Nafikiri ningewaona kweli mna akili na mapenzi ya dhati kwa huyo msanii wenu (Wema) kama mngemshauri apunguze mashoga wapenda anasa na apunguze starehe zisizo na faida, huenda ingemsaidia pesa kuzitumia kwenye kufanya kazi na kuleta maendeleo badala ya kuwapa viwanda vya pombe, mimi kama bwana, wajibu wangu ni kuhakikisha mpenzi wangu anakula vizuri, anavaa vizuri, analala vizuri, na kumuwezesha mtaji wa kufanyia kazi. “Waswahili wanasema mchungaji bora anatakiwa kuhakikisha anampeleka ng’ombe wake kwenye maji safi ila yeye ng’ombe mwenyewe ndiyo anatakiwa aamue kunywa maji!
Aliyekuwa meneja wa Wema, Martin Kadinda.
“Au mnataka nikishampa mtaji niache kufanya na show tena na kuigiza nimuigizie miye? Nisiende studio nikae dukani nimuuzie miye? Ni juhudi zako kwanza! Leo hii hata ningepewa mamilioni ya mamilioni kama nisingekuwa na moyo wa kutaka kujituma na kupenda kufanya kazi yangu, nisingefikia hapa nilipo! Kama nimekuchefua lamba ndimu usitapike.”
WAMGEUKIA DIAMOND
Baada ya waraka huo, mashabiki na wadau waliopo kwenye mtandao huo walimgeukia Diamond kwa kumlaumu kwamba anavyofanya siyo vizuri mbona amemfungulia dada yake Esma Platnumz duka la maana lakini Wema amekuwa akimtumia tu bila faida yoyote?
MARTIN AJIVUA UMENEJA
Kutokana na waraka huo, aliyekuwa meneja wa Wema, Martin Kadinda naye aliandika wa kwake na kutangaza kuachia ngazi ya umeneja kwa mwanadada huyo.
MAMA WEMA AFUNGUKA
Baada ya meneja huyo kubwanga manyanga, wanahabari wetu walimsaka mama mzazi wa Wema, Miriam Sepetu na kumuuliza juu ya mtazamo wake kuhusiana na penzi hilo la mwanaye ambapo alisema kwa sasa penzi hilo limemchosha hivyo anaacha ‘liserereke’.
Alisema kuwa anawaachia wenyewe waendelee kwani ni watu wazima sasa hadi pale atakapohitajika kutoa msaada kama mzazi.
Mama mzazi wa Wema, Miriam Sepetu
“Jamani sitaki mniweke kwenye masuala ya Wema na Diamond, wao wazungushane wee mpaka watakakoamua wenyewe maana wao ni watu wazima.
“Siwezi kuwaingilia, acha liserereke tuone mwisho wake,” alisema mama Wema.
Jitihada za kumpata Wema zilishindikana baada ya simu yake kuita bila kupokelewa, achilia mbali kutojibu ujumbe aliotumiwa katika Mtandao wa WhatsApp huku mmoja wa marafiki zake akisema kuwa ishu hiyo imemchanganya.
TUJIKUMBUSHE
Penzi la Wema na Diamond limekuwa likigubikwa na sarakasi nyingi kila kukicha. Waliwahi kumwagana kipindi cha nyuma kabla ya kurudiana Oktoba, mwaka jana. Kabla ya kurudiana, kijiti cha penzi la Diamond kilikuwa kikishikiliwa na Mtangazaji Penniel Mungilwa ‘Penny’.

0 comments: